UCHAGUZI mdogo wa ubunge Chalinze, Bagamoyo, mkoani Pwani unaofanyika
leo ambapo jumla ya vituo 288 vya kupigia kura vilivyotumika katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 vitatumika tena.
Akizungumzia maandalizi ya uchaguzi huo jana, msimamizi wa uchaguzi
huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo,
Samuel Salianga, alisema maandalizi yamekamilika kwa asilimia 95 na
vifaa muhimu vimesambazwa kwenye vituo hivyo.
Alivitaja vyama vitano vinavyoshiriki uchaguzi huo kuwa ni CCM,
CHADEMA, CUF, NRA na AFP huku akibainisha idadi ya wapiga kura kuwa ni
92,939.
Kwa upande mwingine Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyama
vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa Chalinze kuhakikisha
vinawatumia mawakala wanaotoka eneo la vituo ili wawatambue wapiga kura
wa eneo hilo.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian
Lubuva, alisema sheria haikatazi vyama hivyo kuteua mawakala kutoka
majimbo mengine ya uchaguzi lakini ni vema kuwateua wale wanaotoka eneo
lenye wapiga kura wanaowafahamu.
Licha ya kuwepo kwa idadi hiyo ya waliojiandikisha katika daftari la
kupiga kura lakini kuna wasiwasi wa wapiga kura kutofikia idadi hiyo
kutokana na miundombinu ya baadhi ya maeneo kuharibiwa na mvua
zinazonyesha mkoani hapa.
No comments:
Post a Comment