Kampala. Vikosi vya Marekani kwa ajili ya kumkabili kiongozi wa
kundi la Lord Resistance Army (LRA) Joseph Kony vimewasili nchini Uganda
huku vikiwa na vifaa vya kisasa zikiwamo ndege zenye uwezo wa kujaza
mafuta angani.
Taarifa zimesema kuwa askari hao 150 waliwasili
siku tatu zilizopita na kwamba sasa wanatazamiwa kuanzisha msako mkali
katika maeneo ya mpakani mwa Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati ambako
kiongozi huyo anaaminika kujifisha.
Hivi karibuni Rais Barack Obama aliidhinisha
kutumwa kwa vikosi hivyo kama sehemu ya kuunga mkono juhudi
zilizoanzishwa na Umoja wa Afrika za kumsaka Kony ambaye pia anatakiwa
na mahakama ya kimataifa ya uhalifu(ICC) kutokana na makosa ya uhalifu
dhidi ya binadamu.
Askari hao wamewasili wakiwa na vifaa vya kisasa
ikiwamo ndege aina ya CV-200 yenye uwezo wa kujaza mafuta ikiwa angani
na kwamba mkakati wao wa kwanza ni kuelekea kwenye misitu ya Jamhuri ya
Afrika ya Kati.
Ofisa habari katika ubalozi wa Marekani nchini
Uganda Daniel Travis alithibitisha kuwasili kwa askari hao lakini hata
hivyo hakuwa tayari kutoa maelezo zaidi.
“Hatuwezi kueleza zaidi kuhusiana mahali ambako
vikosi hivyo vipo zaidi ya kusema kwamba vitakuwepo nchini kwa muda
maalumu na hatutarajia kuona vinakuwepo zaidi ya muda
ulioamuliwa,”alisema.
Vikosi hivyo vya Marekani vinatazamiwa kuongeza
nguvu juhudi za kumsaka kiongozi huyo ambaye anatuhumiwa pia kwa
kuwaandikisha askari watoto na kuhusika katika vitendo vya ubakaji.
Kwa muda mrefu vikosi vya Umoja wa Mataifa
vimekuwa vikiendesha msako dhidi ya Kony bila mafanikio yoyote kutokana
na kuhamisha mara kwa mara maficho yake. Vikosi hivyo vya Afrika
vinaundwa na askari kutoka Uganda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasi
ya Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
CHANZO:MWANANCHI
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment