Shule zote katika kisiwa cha Zanzibar zimefungwa kwa muda kutokana na mvua kali ambayo imesababisha mafuriko.
Waziri wa elimu katika kisiwa hicho Riziki Pembe Juma amesema kuwa mvua hiyo ambayo pia imekuwa ikinyesha katika kisiwa cha Unguja na Pemba kwa kipindi cha wiki tatu zilizopita pia imeharibu barabara na mali ya watu.
Alisema kuwa baadhi ya shule zimejaa maji hivyobasi kuwa vigumu kwa walimu kufunza mbali na kuwa wanafunzi wanashindwa kufika kutokana na mafuriko.
Waziri huyo amefichua kwamba uamuzi huo uliafikiwa kufuatia pendekezo kutoka kwa kamati ya kukabiliana na majanga ya Zanzibar ambayo iliishauri serikali kufunga shule hizo kwa usalama wa wanafunzi.
Baada ya kuangazia mapendekezo hayo tulikuwa hatuna njia nyengine bali kuzifunga shule hadi pale hali itakaporudia hali yake ya kawaida.
Hatahivyo amesema kuwa wanafunzi wa kidato cha sita waliokuwa wakifanya mitihani yao ya mwisho wataendelea kufanya hivyo.
Kufikia sasa kuna takriban wanafunzi 364 495 wa shule za msingi na zile za upili zanzibar.
CHANZO: BBC SWAHILI
No comments:
Post a Comment