Hakimu Rwezile alitoa onyo hilo jana kufuatia sintofahamu iliyoibuka mahakamani hapo baada ya baadhi ya askari magereza waliokuwa na silaha kuwafukuza waandishi wa habari wakiwazuia kuchukua picha za mwenendo wa kesi hiyo.
“Hakuna usiri mahakamani, hatutarajii tena kuona misuguano hapa, tayari nimezungumza na waandishi na askari magereza kuhusiana na suala hili, eneo hili lipo chini ya mahakama. Hivyo, watu wanapaswa kuingia na kutoka salama,” alisema Hakimu Rwezile.
Katika kesi ya msingi ambapo Lema alifikishwa mahakamani hapo kwa kesi ya uchochezi inayomkabili. Wakili wa Serikali aliiambia mahakama kuwa tayari ushahidi umekamilika na kwamba upande wa Jamhuri una mashahidi saba ambao wote ni askari polisi.
Wakili wa Serikali aliiambia Mahakama kuwa kati ya Agosti Mosi na 26 mwaka huu Lema alisambaza ujumbe wa sauti kupitia Whatsapp akiwahamasisha watu kufanya maandamano Septemba Mosi, kinyume cha kifungu cha 390 (35) cha Kanuni za Adhabu, kama kilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Hata hivyo, Lema alikana mashataka yote dhidi yake na Hakimu Rwezile aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 2 mwaka huu ambapo mashahidi wataanza kutoa ushahidi wao.
Lema alirudishwa mahabusu akisubiri hatma ya dhamana yake kuamriwa leo na Mahakama Kuu.
No comments:
Post a Comment