Mwanariadha wa Jamaica, Usain Bolt, ameandikisha historia ya kuwa mwanariadha wa kwanza kushinda nishani ya dhahabu kwa mara ya tatu mfululizo, katika mbio za mita mia moja, kwenye michezo ya olimpiki ya Rio 2016.
Bolt, 29, amechukua muda wa sekunde 9.81 katika fainali yake ya mwisho katika michezo ya olimpiki, kwa kuiga ushindi sawa na huo katika michezo ya olimpiki mjini Beijing 2008, na London 2012.
Gatlin, ambaye amepigwa marufuku mara mbili kwa matumizi ya dawa za kutitimua misuli, alimaliza sekunde 0.08 nyumna ya Bolt na kuchukua nishani ya fedha.
"Nilitarajia kwenda kasi zaidi, lakini nafurahia kwamba nimeshinda," Bolt ameiambia BBC.
Mwanariadha wa Canada Andre de Grasse ameshinda nishani ya shaba, na kuandikisha muda bora wa kibinafsi wa sekunde 9.91, mbele ya mwanariadha wa Jamaica Yohan Blake.
Bolt anatazamia kuondoka Rio na nishani zaidi za dhahabu katika mbio za mita 200 na mita 100 kupokezana vijiti, jinsi ilivyokuwa katika michezo ya olimpiki ya mwaka 2008 na 2012.
Mwanariadha huyo anayeshikilia rekodi ya dunia katika mbio za mita 100 alisema kuwa atastaafu kutoka kwenye ulingo wa riadha baada ya michuano ya ubingwa dunia mwaka 2017.(CHANZO:BBCSWAHILI)
No comments:
Post a Comment