UZEMBE HATI YA MUUNGANO: SAINI ZA NYERERE,MSEKWA ZACHEZEWA - ANGA ZA KIMATAIFA

Latest

Tuesday, April 8, 2014

UZEMBE HATI YA MUUNGANO: SAINI ZA NYERERE,MSEKWA ZACHEZEWA


 
 
 
Dodoma. Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta amekiri “kuchezewa” kwa saini ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na sehemu ya saini ya aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius Msekwa zilizopo kwenye hati ya sheria ya kuridhia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Akizungumza na gazeti hili jana, Sitta alisema ni kweli kuna maneno katika hati hiyo ya sheria namba 22 ya 1964, iliyosainiwa na Nyerere na Msekwa, Aprili 25, 1964, yameongezwa. Alisema katika saini ya Nyerere kumeongezwa herufi “us” kwa kompyuta na katika sehemu ya saini ya Msekwa kumeandikwa neno “Msekwa” kwa kompyuta, jambo ambalo ni makosa. Sitta alisema walioongeza maneno hayo ni wafanyakazi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya kuona sehemu ya maandishi kwenye saini hizo hayasomeki, lakini walifanya makosa. “Wale vijana walipoona document (nyaraka) haisomeki waliongeza “us” mwisho kwa kompyuta kwenye saini ya Nyerere, ila walifanya makosa maana bora kitu kionekane kufifia hivyo hivyo lakini kibaki na maana yake,” alisema. Hata hivyo, Sitta alisema kwa waliofanya kazi na hayati Baba wa Taifa wanatambua saini iliyopo kwenye hati ya sheria hiyo ipo sawa ukiondoa makosa ya kuwekwa herufi hizo. Kuhusu saini ya Msekwa, alisema pia kulifanyika makosa katika sehemu ya saini hiyo, kuandikwa kwa kompyuta “Msekwa”. “Ni saini ya Msekwa, lakini vijana wa chamber kwa AG waliongeza neno “Msekwa” kwa kompyuta. Ni mtu asiyejua thamani na uhalisia wa saini ni kubaki ilivyo hata kama kwa miaka 100 hata mtu aje kuisoma kwa darubini,” alisema. Hata hivyo, alisema maudhui ya hati ya sheria hiyo, iliyosainiwa rasmi Aprili 25, 1964 ni sahihi kama ambavyo walikubaliana waasisi wa Muungano, Nyerere na Karume. Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema alisema kwamba hafahamu kama ofisi yake inahusika na kuchezewa kwa saini hizo, tofauti na madai ya Sitta. Sheria iliyopitishwa Z’bar Sitta alisema ili kuondoa utata, ameagiza kupatiwa hati ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume (Presidential Decree) aliyotoa kusaini makubaliano kwani wakati huo, hakukuwa na Bunge. “Karume alitumia Baraza la Mapinduzi akatumia amri ya Rais akasaini. Tunatarajia kuipata hiyo, sasa tutakuwa tumepata nyaraka za Bara na Zanzibar,” alisema Sitta.

No comments: