DALILI ZA VURUGU ZAONEKANA ARUSHA. - ANGA ZA KIMATAIFA

Latest

Tuesday, June 11, 2013

DALILI ZA VURUGU ZAONEKANA ARUSHA.

 
ARUSHA-TANZANIA,
HALI ya vurugu imeanza kujitokeza katika mchakato wa kampeni za uchaguzi mdogo wa nafasi za udiwani katika kata nne za Jiji la Arusha kufuatia matukio ya uvunjifu wa amani baina ya wafuasi wa vyama vya CHADEMA na CCM.

Katika uchaguzi mdogo huo uliopangwa kufanyika Juni 16, mwaka huu, wagombea waliopitishwa, na vyama vyao vikiwa kwenye mabano, ni kata ya Themi, Melance Kinabo ‘Kaburu’ (CHADEMA), Victor Mkolwe (CCM) na Labora Peter Ndapoi (CUF), kata ya Kaloleni ni Emanuel Kessy (CHADEMA), Emanuel Meleari (CCM) na Abbas Darwesh (CUF).
Kata ya Elerai ni Jeremiah Mpinga (CHADEMA), Emanuel Laizer (CCM), John Bayo (CUF), wakati kata ya Kimandolu inagombewa na Reyson Ngowi (CHADEMA) na Edna Jonathan Sauli (CCM).

Hata hivyo, pamoja na vyama hivyo kuendalea na kampeni za kuwanadi wagombea wake, matukio hayo ya vurugu yameshika kasi mwishoni mwa wiki hii baada ya CCM kukilalamikia CHADEMA kuvuruga mkutano wake wa kampeni uliokuwa ukifanyika eneo la Themi-Engira, siku ya Jumapili.

Katika tukio hilo, CCM wanadai kwamba gari la matangazo la CHADEMA aina ya Canter lenye namba za usajili T261AFX, lilipita eneo la mkutano uliokuwa ukiendelea na kitendo ambacho CCM wanadai kusababisha hali ya taharuki kwa wananchi waliohudhuria.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo ambalo lilitokea majira ya saa nane mchana, wamesema kufuatia tukio hilo vijana waliokuwa wanalinda mkutano wa CCM, walivamia gari hilo na kulipiga mawe na kuvunja vioo, pamoja na kuharibu spika za matangazo kwa kukata nyaya.
“Baadaye wafuasi wa CHADEMA nao waliwasili eneo hilo na kuanza kupambana na wale wa CCM hadi polisi walipoitwa kunuru hali iliyojitokeza,” aliongeza mmoja wa mashuhuda hao.
Hata hivyo, taarifa zinadai kuwa kufuatia tukio hilo, idadi kubwa ya watu iliondoka katika mkutano huo wa CCM wakihofia usalama wao kutokana na vurugu hizo.

Viongozi wa CCM wamemtuhumu mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema aliyekuwa ameandamana na wapambe wake katika eneo hilo, akidaiwa kuwa chanzo cha vurugu hizo kwa maelezo kwamba wafuasi hao wa CHADEMA walivuruga mkutano huo kwa maelekezo ya mbunge huyo.

Katika tukio jingine, kada mmoja wa CCM, Victor Mollel, anadaiwa kumtishia kwa silaha ya moto (bastola) Katibu wa CHADEMA, Kata ya Kaloleni, Ally Ogaga, mbele ya Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Arusha, na hivyo polisi kulazimika kumweka selo kwa muda.
Aidha, katika tukio jingine lililotokea Jumamosi iliyopita katika eneo la Kaloleni, watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa CCM walishambulia gari la matangazo la CHADEMA na kuliharibu kwa kuvunja vioo.

Bulembo awashukia polisi
Kufuatia vurugu hizo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa, Alhaji Abdalah Bulembo, amelishukia Jeshi la Mkoa wa Arusha na kuahidi kuwashitaki askari wa jeshi hilo wa ngazi zote kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa kufanya kazi zao kwa upendeleo wa kisiasa.

Akimnadi mgombea wa CCM katika uzinduzi wa kampeni hizo kata ya Themi, Victor Mkolwe, Mwenyekiti huyo wa Wazazi, alilituhumu jeshi la polisi mkoani Arusha kwa kile alichodai kuonyesha udhaifu katika utendaji wao wa kazi, ikiwa ni pamoja na kushindwa kuwakamata viongozi wa CHADEMA, na hasa mbunge Lema ambaye alikuwa kinara wa vurugu.

Kabla mkutano huo wa Jumapili, Jumamozi iliyopita Bulembo pia alimnadi na kuzindua kampeni za CCM za mgombea wa kata ya Kaloleni, Emanuel Meliari.
“Leo usiku, Waziri Mkuu Mizengo Pinda atawasili jijini Arusha kwa ajili ya ufunguzi wa mkutano wa maji unaowakutanisha wakurugenzi wa majiji, halmashauri zote nchini pamoja na wakurugenzi wa mamlaka za maji nchini, naahidi kwamba suala la utendaji wa polisi nitawasilisha kwake,” alisema Bulembo.

Mwenyekiti huyo wa Wazazi alieleza kuwa suala la kupewa ulinzi katika mikutano ya kampeni liko kisheria na askari kuwapatia wananchi ulinzi pamoja na mali zao si suala la kuomba, bali ni wajibu wa polisi na kwamba kushindwa kutekeleza majukumu wao huo, ni kuzembea kazi.

“Kimsingi nitamshauri Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu kufanyika kwa mabadiliko ya askari wa jeshi hilo mkoani Arusha, kuanzia wale wa vyeo vya juu hadi chini ili kuleta ufanisi katika jeshi hilo ambalo linategemewa kutoa ulinzi siku ya uchaguzi,” alisema Bulembo na kuongeza:
“Sisi ndiyo Chama Tawala. Tuna dola na kila kitu, sasa tunaweza tukaamua tu kuwaondoa askari wote hapa Arusha, tukaleta kikosi kazi kingine kifanye kazi, nyie wengine wote mmeshakua mashabiki wa CHADEMA na wewe OCD upo hapo, nakutuma ukamueleze bosi wako.
“Wito wangu kwa wanasiasa wenzangu, ni kwamba Utanzania utangulie mbele ya vyama vyetu. Hizi vurugu za kisiasa hazitatufikisha popote, tujiulize kwa kufanya vurugu tunawarithisha nini watoto wetu?”

Kutokana hali ya Arusha kugeuka kuwa kitovu cha vurugu za kisiasa nchini, Bulembo alibainisha kuwa hata Rais wa Marekani, Barack Obama ambaye atawasili nchini kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu, amekwepa kutembelea mji huo kutokana na vurugu za mara kwa mara.
“Kutokana na vurugu za kisiasa zinazojitokeza kila wakati,  Arusha si sehemu salama tena na ndiyo maana hata Rais wa Marekani, Barack Obama amekwepa kufika katika mji ambao awali kila kiongozi wa Taifa lolote duniani anayekuja Tanzania hutembelea, ikiwa ni pamoja na vivutio vya utalii,” anasema.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, alisema vurugu hizo zimeathiri kwa kiwango kikubwa mikutano yao kampeni, akitolea mfano wa siku hiyo ya vurugu ambapo mkutano wao, badala ya kuanza saa 7.30 hadi 8.00 mchana, ulilazimika kuanza saa 10.30 jioni.

Aidha, alisema mbali na athari hizo, pia wapo vijana wa chama chake ambao walijeruhiwa kutokana na vurugu hizo zinazodaiwa kuongozwa na Lema aliyepita na gari kubwa la matangazo katika eneo hilo la mkutano wakati chama chake hakikuwa na ratiba ya mkutano katika eneo hilo.

CHADEMA wajibu mashambulizi
Akijibu madai hayo ya CCM, mbunge wa Arusha Mjini, Lema, alisema madai hayo ni uzushi mtupu na yamelenga kuwachafua mbele ya jamii.

“Ni kweli gari letu la matangazo lilipita eneo hilo, lakini gari lilipita barabarani kuelekea Themi-Kambarage. Kama CCM wana mkutano eneo moja, haina maana kwamba sisi tusifanye kampeni zetu eneo jingine,” alisema Lema.

Alisema kuwa akiwa katika mkutano wa kanda wa chama chake, alipigiwa simu na vijana waliokuwa kwenye gari hilo la matangazo, lakini kabla ya kwenda eneo la tukio, walipita polisi na kuandamana nao hadi eneo la tukio ambapo walikuta vurugu zinaendelea.
“Polisi na mimi tulisadiana kutuliza zile vurugu. Sasa nawashangaa viongozi wa CCM wanaotaka mimi nikamatwe na kuhojiwa. Kwa kweli siwaelewi CCM na viongozi wao naona sasa wanataka Lema asiishi kabisa,” alisema.
Lema alisema kauli za viongozi wa CCM ni ushahidi tosha kuwa chama hicho sasa kinatapatapa na kuomba huruma ya vyombo vya dola badala ya kujenga hoja katika majukwaa ya kisiasa. Alisema CCM kitashindwa vibaya katika uchaguzi mdogo huo utakaofanyika Juni 16 mwaka huu katika kata zote hizo nne.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Arusha Mjini, Ephata Nanyaro, alisema taarifa za viongozi wa CCM kwamba chama chake kimevuruga mkutano wao, ni uzushi mtupu, huku akiwata wananchi kuwapuuza.
“Baada ya kupata taarifa hizo za vurugu, sisi ndio tuliokwenda polisi pamoja na mbunge wetu, na tuliambata na polisi hadi eneo la tukio, na sote kwa pamoja tulisadiana kurejesha hali ya amani…sasa nawashangaa sana wanapodai eti tulivuruga mkutano wao.” alisema Nanyaro.

Kabla ya matukio hayo ya vurugu, Nanyaro anasema wao kama CHADEMA waliandika barua kwenda polisi kuarifu juu ya taarifa za uhalifu wa kuvuruga mikutano ya kampeni ya chama chao zilizopangwa kufanywa na makada wa CCM, hali iliyowafanya polisi kuitisha mkutano wa pamoja wa viongozi wa vyama vyote ili kuweka mambo sawa.
Kwa mujibu wa Nanyaro, mkutano huo baina ya polisi na viongozi wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi mdogo huo, ulifanyika katika ofisi za kamanda wa polisi wilaya (OCD) wiki iliyopita.
CUF nao watoa kauli
Wakati CCM na CHADEMA wakifanyiana rafu, kwa upande wake Chama cha Wananchi (CUF) kimeendesha kampeni za kuwanadi wagombea wake kwa njia za kistaarabu, huku kukiwa na habari kwamba wagombea wa chama hicho wanatoa upanzani mkali kwa wagombea wa vyama vikuu hivyo katika siasa za Arusha, na hasa katika kata za Elerai na Kaloleni.

Katika mkutano wao wa kampeni uliofanyika kata ya Elereai, mgombea wa CUF, John Bayo, ambaye ni kati ya madiwani wa CHADEMA waliofukuzwa mapema mwaka jana, aliwaomba wananchi wa kata hiyo wampe kura zao kwa kuwa mgombea wa CHADEMA hawezi kuwawakilisha katika Baraza la Madiwani kwa sababu wamesusia vikao hivyo.

“Kama CHADEMA hawahudhurii vikao vya Halmashauri, je; mnampigia kura mgombea wake kwa sababu zipi? Hakuna sababu ya kupoteza kura zenu kwake kwani hatahudhuria vikao vya Halmashauri na kushiriki katika mipango yenu ya maendeleo,” alisisitiza Bayo.(CHANZO:RAIA MWEMA)

No comments: