Mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, umesababisha mazingira magumu kwa Madaktari na wafanyikazi wa misaada ya kibinadamu kuwafikia waathirika na watu wengine.
Shirika la afya duniani WHO linasema watu 9 wameambukizwa na ugonjwa huu hatari na tayari watatu wamepoteza maisha katika mkoa wa Bas-Uele.
Kutokana na miundo mbinu mibaya kama barabara, watalaam wa afya wanasema imekuwa ni vigumu sana kuwafikia watu hao jambo ambalo linahatarisha uharaka wa kuudhibiti ugonjwa huo hatari.
Eneo hilo lina barabara nyembamba ambazo zinapita katikati ya misitu katika mkoa huo.
Hata hivyo, WHO inasema inashirikiana kwa karibu na serikali ya DRC kuhakikisha kuwa wanafanikiwa kudhibiti ugonjwa huo.
Mara ya mwisho kwa Ebola kulikumba taifa hilo, ilikuwa ni mwaka 2014 na kusababisha watu 49 kupoteza maisha lakini baadaye maafisa wa afya wakafanikiwa kuudhibiti.
Ugonjwa huu ulisumbua sana Mataifa ya Magharibi mwaka 2013 na kusababisha vifo vya watu 11,300 na kuwambukiza wengine nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia.
Dalili za Ebola ni pamoja na homa kali, kuumwa kwa misuli ya mwili, kuharisha, kutapika, kutokwa kwa damu kutoka maeneo yaliyo wazi ya mwili.
Mtu anaweza kuambukizwa kwa kumshika mnyama aliyeambukizwa, mtu aliyeambukizwa kupitia majimaji ya mwili wake ikiwa ni pamoja na damu.
Watalaam pia wanashauri kuwa mtu aliyefariki duniani kwa sababu ya Ebola asisogelewe wala kuguswa.
No comments:
Post a Comment