RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesaini muswada wa utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ambao sasa utaipa ruhusa Zanzibar kisheria kutafuta nishati hiyo kwa maslahi ya Zanzibar na wananchi wake.
Utiaji saini huo ulifanyika Ikulu na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Dk Shein alisema rasilimali ya mafuta na gesi asilia ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa kwenye orodha ya Muungano ambayo usimamizi wake kabla ya kutungwa kwa Sheria Namba 21 ya 2015 ilikuwa chini ya Shirika la Maendeleo la Mafuta (TPDC) pamoja na Sheria ya Utafutaji na Uzalishaji wa Mafuta, Sura ya 328, sheria ambayo ilikuwa inatumika pande zote mbili za Muungano.
Hata hivyo, alisema mfumo huo uliokuwepo ulionekana kuwa na upungufu na kubwa zaidi mfumo huo ulikuwa hautoi fursa kwa SMZ na watu wake katika kusimamia rasilimali ya mafuta na gesi asilia. Pia, haukutoa fursa kwa Zanzibar katika muundo wa kiutawala wa taasisi zinazosimamia utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia.
Alisema kwa sababu suala la mafuta ni uchumi, SMZ ilipendekeza kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa suala la mafuta na gesi asilia liachiwe kila upande wa Muungano kusimamia rasilimali hiyo pamoja na mapato yake.
Hata hivyo, suala la mafuta na gesi asilia halijaondoka kwenye Katiba ya Muungano, Sheria ya Bunge imetambua hilo na imeweka usimamizi wa rasilimali hiyo kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kusainiwa kwa sheria hiyo sasa inafungua milango kwa kampuni na taasisi mbalimbali zenye nia ya kuchimba mafuta na gesi asilia kwenda Zanzibar kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo.
No comments:
Post a Comment