Maofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Juma Matandika na Martine Chache, leo Jumatano wamepandishwa kwenye Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam wakituhumiwa kuomba rushwa ya shilingi milioni 25 kwa timu ya soka ya Geita Gold ili kuisaidia kupanda daraja.
Wahusika hao walifikishwa mahakamani hapo mapema na baadaye walipandishwa kizimbani kwa tuhuma hizo ambapo inadaiwa walitenda kosa hilo Februari 4, mwaka huu kwenye ofisi za TFF zilizopo Karume jijini Dar.
Juma Matandika |
Kesi hiyo ambayo ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi Huruma Shahidi ilisimamiwa na wakili Leonard Swai akiwakilisha upande wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wakati upande wa serikali iliwakilishwa na wakili Odesa Horombe. Upande wa watuhumiwa walitetewa na wakili Claudia Nestory.
Katika tuhuma hizo, watuhumiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo kwa kuomba rushwa kwa viongozi wa Geita Gold, Salum Kulunge na Costantine Molandi kwa ajili ya kushinikiza TFF wawapandishe Ligi Kuu Bara kutoka Ligi Daraja la Kwanza katika ligi ya msimu uliopita.
Mara baada ya kusomewa mashtaka hayo, watuhumiwa wote walikana kutenda kosa hilo ambapo kesi imeahirishwa hadi Novemba 30, mwaka huu, watuhumiwa wote wameachiwa kwa dhamana ya shilingi milioni 5 kila mmoja.
No comments:
Post a Comment