Mikataba hiyo imegusa nyanja za Gesi, huku ombi lake la Tanzani kujengewa uwanja wa kisasa mjini Dodoma likikubaliwa na Mfalme huyo.
Uwanja huo utakaogharimu dola 80 hadi 100( zaidi ya bilioni 171) utajengwa Dodoma na unategemewa kuwa mkubwa zaidi kuliko ule wa Taifa.
MAMBO MENGINE KATIKA MIKATABA:
katika kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili kwenye nyanja ya usalama na ulinzi, Mfalme huyo amekubali kuanzisha programu ya kubadilishana mafunzo baina ya askari wa Tanzania na Morocco na kwa kuanza wiki ijayo askari 150 wa Tanzania watakwenda mafunzoni nchini Morocco.
Katika
ziara ya siku tatu ya kikazi ya Mfalme Mohammed VI aliyewasili nchini
juzi, akiwa na ujumbe wa wafanyabiashara pamoja na viongozi wengine,
wamefanikiwa kufanya makubaliano ya mikataba 21 katika nyanja mbalimbali
zikiwamo za kilimo, gesi, madini na na usafiri wa anga.
Mikataba
hiyo ni pamoja na Makubaliano ya Jumla katika Ushirikiano wa Uchumi,
Sayansi, Ufundi na Utamaduni baina ya Serikali ya Morocco na Tanzania
yaliyosainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga na Waziri wa wizara hiyo wa
Morocco, Salahddine Mezouar.
Mwingine
ni ule wa kuanzishwa kwa Jukwaa la Mashauriano ya kisiasa baina ya
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na wizara hiyo
nchini Morocco, mkataba wa ushirikiano kwenye sekta ya gesi, nishati,
madini na sayansi ya miamba, mkataba wa ushirikiano wa usafiri wa anga,
mkataba wa ushirikiano kwenye mradi wa mtangamano wa kuwasaidia wakulima
wadogo nchini.
Pia
mkataba wa makubaliano kwenye sekta ya uvuvi, mkataba wa makubaliano
baina na MASEN-Morocco na Wizara ya Nishati na Madini kwa ajili ya
maendeleo ya nishati mbadala, mkataba wa ushirikiano baina ya Shirika la
Mbolea la Morocco (OCP) na Shirika la Mbolea la Tanzania katika
kuendeleza soko la mbolea na kilimo nchini.
Pia
mkataba baina ya Bodi ya Utalii Tanzania na Kamisheni ya Utalii
Zanzibar na Ofisi ya Utalii ya Taifa nchini Morocco, Mkataba wa Kundi la
Utoaji Mikopo la Morocco na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania,
Mkataba baina ya Shirika la Bima la Taifa (NIC) na Shirika la Bima la
Morocco.
Mingine
ni Mkataba wa Maeneo Maalumu ya Uwekezaji (EPZA) na Kundi la SNTL la
Morocco katika ubia wa uendelezaji na utangazaji wa viwanda, mkataba wa
usafirishiaji kwenye reli kupitia Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli
Tanzania (RACO) kwa ajili ya ubia kuendeleza reli ya
Mtwara-Mchuchuma/Liganga.
Aidha,
mkataba mwingine ni ule wa kuanzishwa kwa Baraza la Biashara baina ya
Shirikisho la Wafanyabiashara wa Morocco (CGEM) na Taasisi ya Sekta
Binafsi Tanzania (TPSF), Mkataba wa Mkopo baina ya Benki ya Afrika (BOA)
na Hospitali ya CCBRT na mkataba wa mkopo wa BOA na Kampuni ya gesi ya
Lake.
Mkataba
wa Mkopo wa BOA na Kampuni ya Superstar Forwarders, Mkataba wa
Ushirikiano baina ya Kampuni ya OLAM Tanzania na Benki ya Attijariwafa,
mkataba wa ubia baina ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)na Benki ya
Centrale Populaire ya Morocco, mkataba wa Kitaalamu baina ya Shirikisho
la Bima la Morocco na kampuni za bima Tanzania.
Pia mkataba wa ushirikiano baina ya kampuni ya kuchanganya chai ya Morocco na Kampuni ya Afri Tea and Coffee ya Tanzania.
Akizungumzia
MoU kwenye usafiri wa anga, Rais Magufuli alisema wamekubaliana nchi
hizo mbili kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwenda Rabat,
mji mkuu wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
“Na
sisi tumeanzisha shirika letu kidodokidogo linasuasua, lakini tutakuwa
na ushirikiano mzuri na Shirika la Ndege la Morocco, na makubaliano haya
yote ni mwelekeo nzuri wa kuijenga Tanzania na kuwa na uchumi unaokua
kwa asilimia 7.2,” alisema Rais Magufuli.
Rais
Magufuli alisema Morocco imepiga hatua kubwa kwenye utalii na kwamba
mwaka 2015 ilipokea watalii milioni 10.5 na mwakani wanategemea kupokea
watalii zaidi ya milioni 14 na kwamba Tanzania imeshaini makubaliano
kwenye sekta hiyo kwa lengo la kuendeleza hifadhi za nchi na kuutangaza
utalii.
Aidha,
alisema makubaliano yote hayo yamelenga kuijenga Tanzania kuwa nchi ya
uchumi wa kati wa viwanda na kwamba hilo linawezekana kwa kuwa hata sasa
hali ya uchumi wa nchi ni nzuri kwa kuwa unakua kwa asilimia 7.2; na
taarifa za uchumi zinaonesha kwenye robo ya pili ya mwaka uchumi umekua
kwa asilimia 7.9.
“Tuko
kwa ajili ya kuujenga uchumi na niwakaribisheni wageni wetu kutoka
Morocco, niwahakikishieni kuwa mko salama na karibuni kuwekeza kwa faida
ya nchi hizo mbili ambazo uhusiano wake ulianza tangu enzi za Iban
Batutu wa Morocco aliyetembelea Kilwa miaka mingi iliyopita,” alieleza Rais Magufuli.
No comments:
Post a Comment