MPINZANI WA MNYIKA AKUBALI YAISHE. - ANGA ZA KIMATAIFA

Latest

Saturday, December 8, 2012

MPINZANI WA MNYIKA AKUBALI YAISHE.


DAR ES SALAAM-TANZANIA, ALIYEKUWA mgombea Ubunge katika Jimbo la Ubungo, Dar es Salaam, katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, kupitia CCM, Hawa Ng’humbi amebwaga manyanga na kuachana na rufaa ya kupinga ushindi wa John Mnyika (Chadema).

Rufaa hiyo ya kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliothibitisha ubunge wa Mnyika, ilikuwa ianze kusikilizwa jana na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani; Nathalia Kimaro, Salum Massati na Catherine Oriyo.

Mahakama ya Rufani ilikubali kuondolewa mahakamani hapo kwa rufaa hiyo bila gharama, baada ya mkata rufaa kufikia makubaliano na Mnyika nje ya Mahakama.

Uamuzi wa kuiondoa mahakamani rufaa hiyo ulitolewa jana na kiongozi wa jopo la majaji, Jaji Kimaro muda mfupi kabla ya kuanza kusikilizwa kwake. Kabla ya uamuzi huo wa mahakama, Wakili wa Serikali Mkuu, Obadia Kameya alisema walikuwa tayari kwa usikilizwaji.

Hata hivyo, wakili wa Ng’humbi Issa Maige aliieleza Mahakama kuwa mrufani (Ng’humbi) na Mrufaniwa wa pili (Mnyika), wamekubaliana nje ya Mahakama kuiondoa kesi hiyo bila gharama. “Ni kweli rufaa hii ilikuja kwa ajili ya kusilizwa leo, lakini siku mbili zilizopita, mrufani na mjibu rufaa wa pili, walikutana na kuzungumza na kukukubaliana kuiondoa mahakamani bila gharama,” alisema Wakili Maige na kuongeza: “Hivyo chini ya Kifungu cha 102 (3) na (4) cha Kanuni za Mahakama ya Rufani, ninaiomba Mahakama iiondoe rufaa hii, bila gharama.” Mahakama hiyo ilikubali maombi hayo.

Kwa uamuzi huo, Mnyika ataendelea kuwa Mbunge wa Ubungo hadi atakapomaliza kipindi chake mwaka 2015.

Uamuzi huo ulipokewa kwa shangwe na wafuasi cha Mnyika na Chadema kwa jumla, ambao alizungumza nao kuhusu mikakati yake baada ya kesi hiyo kumalizika. Baada ya mazungumzo hayo Mnyika na wafuasi hao waliamua kuondoka mahakamani hapo kwa kutembea kuelekea ofisi za chama hicho, Kinondoni.

Nje ya Mahakama
Akizungumzia uamuzi uliofikiwa baina ya mteja wake, Ng’humbi, Wakili Maige alisema ni hatua nzuri kwa kuwa inakwenda sambamba na sera ya nchi ya kutaka kupunguza mashauri mahakamani. Alisema baada ya Ng’humbi kutafakari na kuangalia muda uliobakia kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao, aliamua kukubalina na Mnyika nje ya Mahakama ili kuiondoa mahakamani rufani hiyo, huku akisema kuwa hatua hiyo pia inaondoa usumbufu na kuokoa muda wa Mahakama.

Mnyika kwa upande wake, alisema siku chache zilizopita Wakili huyo wa Ng’humbi alimpigia simu wakili wake, Edson Mbogoro akimweleza kuwa mteja wake angependa wakutane wazungumze ili waiondoe mahakamani rufani hiyo na kwamba kusiwe na malipo ya gharama za kesi.

Alisema uamuzi huo umethibitisha kuwa ushindi wake ulikuwa ni halali na kwamba sasa atafanya kazi bila wasiwasi.
“Nilipopata taarifa hizo tukashauriana nikaona ni jambo jema kusamehe. Hivyo tumesamehe gharama zote za kesi katika ngazi ya rufaa,” alisema Mnyika.

Hata hivyo, alisema msamaha huo hauhusu gharama za kesi ya Mahakama Kuu kwa kuwa ilishauriwa lakini akasema hata hilo linazungumzika ikiwa Ng’humbi ataomba hivyo.
Mnyika hakubainisha ni gharama kiasi gani alikuwa ametumia katika kesi hiyo akisema ni mpaka pale watakapofanya mchanganuo.

Kwa upande wake, Wakili Mbogoro alisema mbali na gharama nyingine katika kesi ya msingi, tayari kuna Sh9 milioni walizoziweka mahakamani kama dhamana ya kesi.(CHANZO:MWANANCHI)

No comments: