HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) inakabiliwa na upungufu wa
madaktari bingwa wa upasuaji, hususan katika kitengo cha watoto
wanaougua maradhi ya saratani (cancer surgeons).
Upungufu huo unaelezwa umetokana na baadhi ya madaktari bingwa
waliokuwapo awali kufariki dunia mwaka jana, baadhi kuacha kazi na
wengine kustaafu.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini madaktari bingwa wawili walifariki
dunia mwaka jana, ambao ni Dk. Enock Sayi na Dk. Profesa Primo
Carneiro, wakati Dk. Catherine Mng’ong’o anaelezwa kuacha kazi, huku
Dk. Petronella Ngiloi akistaafu kwa mujibu wa sheria.
Habari zilizopatikana hospitalini hapo na kuthibitishwa na mamlaka
husika, ikiwamo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, zinasema mbali na
hospitali hiyo Kuu ya Taifa kukabiliwa na upungufu wa madaktari bingwa,
inakabiliwa pia na tatizo la ukosefu wa mashine za oksijeni za kisasa
za ukutani.
Mashine za oksijeni zilizopo zinadaiwa kufanya kazi chini ya kiwango kinachotakiwa.
Lakini msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris
Mwamwaja, pamoja na kukiri kuwapo kwa upungufu huo wa madaktari
bingwa, amesema hilo haliwezi kuathiri shughuli za tiba katika kitengo
hicho cha magonjwa ya watoto.
Aidha, anasema hospitali hiyo imesheheni vifaa vya kisasa, zikiwamo
mashine hizo za oksijeni, zinazotumika kumsaidia mgonjwa kupumua.
Uchuguzi uliofanywa na gazeti hili katika Jengo la Watoto na kwenye
baadhi ya wodi za Hospitali ya Taifa Muhimbili, umebaini pia kuwapo kwa
vichwa vya mashine za mitungi ya oksijeni vikiwa vimezungushiwa plasta
kuzuia uvujaji hovyo wa hewa hiyo, hali inayohatarisha afya za
wagonjwa wanaolazwa katika wodi zenye mashine hizo.
“Hayo mambo yanashughulikiwa na Bodi ya Muhimbili pamoja na
Mkurugenzi wake. Kama masuala hayo unayouliza yatahitajika kufika
wizarani, ndipo hapo na sisi tunaweza kutolea ufafanuzi, lakini
ninavyojua Muhimbili kuna vifaa vyote vya kisasa na ndiyo maana imeitwa
Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Muhimbili,” alisema Mwamwaja.
Mmoja wa madaktari bingwa wa Muhimbili, ameliambia gazeti hili kwamba
tangu walipofariki madaktari bingwa wenzake; Dk. Sayi na Profesa
Carneiro mwaka jana, nafasi zao hadi sasa hazijajazwa.
Aidha, daktari bingwa huyo ambaye hakupenda jina lake litajwe kwa
sababu zilizo wazi kabisa, amethibitisha kuwapo kwa tatizo la madaktari
bingwa katika kitengo cha saratani, baada ya Dk. Ngiloi kustaafu.
Alisema awali baada ya Dk. Ngiloi kustaafu, Dk. aliyechukua nafasi
yake hiyo katika kitengo hicho alikuwa Dk. Mng’ong’o, lakini kwa sasa
anadaiwa kuacha kazi hospitalini hapo.
No comments:
Post a Comment