IRINGA-TANZANIA
Watu saba wanaosadikiwa kuwa
majambazi wakiwa na silaha za moto wamevamia Kanisa Katoliki Parokia ya
Isimani mkoani hapa linaloongozwa Rais wa Baraza Kuu la Maaskofu wa
kanisa hilo (TEC), Askofu Tacius Ngalalekumtwa na kisha kupora fedha
zaidi ya Sh.milioni 2.5 na kuwajeruhi kwa risasi mapadre wawili.
Tukio hilo limekuja siku moja tu baada ya watu wengine wanaosadikiwa
kuwa majambazi kuvamia Kanisa Katoliki Parokia ya Kihesa Jimbo la
Iringa mjini ambao walipora vitu mbalimbali na kumjeruhi kwa risasi
mlinzi wa kanisa hilo.
Katika tukio la uvamizi wa kanisa la Parokia ya Isimani, mapadre
waliojeruhiwa kwa kupigwa risasi ni Padre Angelo Burgio raia wa
Italiano, na Helman Myala ambaye ni paroko wa kanisa hilo aliyejeruhiwa
kwa kupigwa mapanga sehemu kadhaa za mwili wake.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Mkoa, Padre
Angelo Burgio, alisema walivamiwa na watu saba walikuwa na silaha za
moto na za jadi majira ya saa 4:30 usiku ambao walivunja milango ya
kuingilia ndani.
“Waliotuvamia walikuwa saba wakiwa na bunduki, virungu, nondo na
mapanga wakatuamuru tuwaoneshe pesa zilipo, wakaanza kunipiga kwa
virungu huku mmoja akiniwekea bunduki tumboni kisha wakachukua zaidi ya
Sh. 2,500,000,”alisema Padre Burgio.
Alisema mwenzake Padre Myala walinyang’anya kiasi cha Sh.1,300,000 na simu za mikononi.
Hata hivyo alisema hajui mali zingine zilizochukuliwa kwa kuwa baada ya
kuvamiwa na kuumizwa hawakupata nguvu tena za kuweza kukagua vitu
vingine.
“Kwa kweli sijui uharibifu mwingine kwa sababu baada ya kuvamiwa na
kuumizwa hatukupata nguvu tena ya kuweza kukagua vitu vingine ndipo
tulipokimbizwa na wasamalia wema hospitalini” alisema.
Kaimu wa Mganga Mkuu wa hospitali ya Mkoa wa Iringa Dk.Gwanchele Faustine amekiri kupokea majeruhi hao majira ya saa 7 usiku.
“Tumepokea majeruhi wawili usiku ambao ni Mapadre wa Kanisa katoliki
Padre Angelo Burgio na Padre Helman Myala, Padre. Angelo amepigwa
risasi upande wa kushoto na kutokea upande wa kulia lakini kuna risasi
zingine zipo kifuani tunamuandaa aingizwe kufanyiwa upasuaji sasa hivi”
alisema Dk.Faustine.
Hata hivyo alisema pamoja na matibabu wanayoendelea kupata hali zao zinaendelea vizuri.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kihorogota, Costantino Kihwele,
alisema vijana wameingia kwenye msako kila sehemu na kufanikiwa
kumkamata kijana mmoja anayesadikiwa kuwa ni mmoja wa tukio hilo akiwa
na bunduki.
“Kuna kijana mmoja amekamatwa na vijana wa Isimani ambao waliamua
kuingia msituni kufanya msako lakini jina lake nitakwambia kadiri
tutakavyokuwa tunaendelea na msako” alisema.
Katika hatua nyingine, Dk. Faustine alisema mlinzi wa Kanisa la Kihesa aliyejeruhiwa jana hali yake bado ni mbaya.
“Mlinzi wa Kanisa la Kihesa aliyejeruhiwa na kufikishwa hapa bado hali yake ni mbaya na bado tunaendelea kumhudumia” alisema.
Juzi Kanisa Katoliki Parokia ya Kihesa Jimbo la Iringa lilivamiwa na
kuvunjwa milango na watu wasiojulikana huku mlinzi Bathlomeo Nzigilwa
akijeruhiwa kwa risasi.
Akitoa maelezo juu ya tukio hilo kanisani hapo, mhuduma wa Kanisa hilo
Sista Lucy Grace Mgata alisema aligungua kuwa kunauvamizi umefanyika
alfajiri alipofika kanisani hapo kwa ajili ya kufungua milango ya
Kanisa tayari kwa Ibada ya Misa za kila siku zinazoanza saa 12:00
asubuhi.
“Nilifika hapa saa 11:40 alfajiri kwa ajili ya kufungua milango na
kufanya maandalizi kwa ajili ya misa lakini nilipoukaribia mlango huo
nikakuta mlinzi amekaa kwenye kiti huku kichwa chake kikiwa
kimeinamishwa chini na kufunikwa kofia nikajua amelala lakini milango
ikawa wazi.
Sista Mgata alisema alipomkaribia mlinzi huyo alikuta damu inamtiririka na ndipo alipokwenda kutoa taarifa kwa padre.
Alisem pamoja na kuvunjwa na uharibifu wa Kanisa hilo, ofisi ya parokia
nayo ilivunjwa huku vitabu, mafaili mbalimbali pamoja na nyaraka
mbalimbali zikiwa zimechanwa na kuvurugwa ovyo kiasi cha kutotamanika.
Mavazi ya ibada na vifaa mbalimbali vya ibada vimeharibiwa vibaya,
Taberenakulo ndogo nayo ikiharibiwa, msalaba kuvunjwa pamoja na Hostia
Takatifu kutupwa kila mahali.
Sista Mgata alisema kuwa kuliwa na hela za watumishi wa artare
walizokuwa wakichangishana kwa ajili ya matumizi ya umoja wao pamoja na
hela za chama cha kitume cha utume wa Fatima zimechukuliwa japo bado
hazijajulikana jumla yake huku funguo za teberenakulo kubwa wanayohidhi
Ekaristi Takatifu zikipoea.
Kwa upande wake Katekista Agustino Luhama mhudumu wa ofisi ya Parokia
alisema hela anazozikumbuka kwa harakaharaka ambazo zimechukuliwa
nawavamizi hao ni zaidi ya shilingi laki tano.
“Hela ninazozikumbuka kwa harakaharaka ambazo zimechukuliwa ni zaidi ya
Sh. 500,000 lakini zingine sijapata idadi kwa sababu nilikuwa
sijazijumlisha na zingine nilizipokea juzi kutoka kwa waamini
mbalimbali” alisema Kat. Luhama.
Padre Aloyce Mdemu ambaye pia ni Makamu wa Askofu wa jimbo hilo alisema
bado ni mapema kujua thamani ya uharibifu uliofanyika kwa kuwa bado
wanaendelea na uchunguzi wa vifaa vingine na maeneo mengine ambayo
huenda hayajagundulika.
Kufuatia matukio hayo ambayo yamelenga makanisa, hali hiyo imezua hofu
kubwa kwa wananchi wa mkoa wa Iringa mbao wamekuwa wakijiuliza kuna
jambo ambalo limejificha kwa kuwa siyo jambo la kawaida kuvamiwa kwa
makanisa na kujeruhi mapadre.
Sunday, November 18, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment