SHEIN AZUNGUMZIA VURUGU ZANZIBAR. - ANGA ZA KIMATAIFA

Latest

Friday, June 1, 2012

SHEIN AZUNGUMZIA VURUGU ZANZIBAR.

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akizungumza katika mkutano na wahariri na waandishi wa vyombo vya habari nchini uliofanyika Ikulu, kisiwani Unguja, jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

BAADA ya kuwa kimya tangu kutokea machafuko Tanzania Visiwani takriban wiki moja iliyopita, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, amejitokeza kuyazungumzia kwa kuonya kwamba, Serikali yake haitavumulia watakaovunja amani huku akiahidi kuimarisha ulinzi kwa wananchi wake.

Kwa siku takriban nne tangu Jumamosi ya wiki iliyopita, visiwa vya Zanzibar viligubikwa na hali tete kiusalama baada ya kuwapo matukio ya uchomaji moto makanisa yanayodaiwa kufanywa na wafuasi wa Jumuiaya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam (JUMIK), ikitaka visiwa hivyo viwe dola huru.

Hatua hiyo ya Rais Shein kujitokeza jana pia imekuja ikiwa ni siku moja tangu jopo la viongozi wa dini ya Kikristo kutoa tamko kali kwa Serikali, wakiitaka iwajibike kwa uharibifu huo uliodumu tangu mwaka 2001.

Jana, akizungumza  na waandishi wa habari Ikulu ya Zanzibar, Dk Shein alisema amesikitishwa na matukio hayo ya Mei 26.

“Mei 26 hapa Zanzibar kulitokea vitendo vya kuvunja amani. Tumeshuhudia maandamano yenye sura ya kidini na jumbe za kisiasa. Mahubiri haya ndiyo yaliyokuwa chachu ya yote haya yaliyotokea,” alisema Dk Shein na kuongeza:

“Jumuiya hizi hazikujali sheria wala utamaduni wa Mzanzibari. Badala yake wakachoma moto majengo, mali na makanisa ya ndugu zetu wakristo na kutoa kauli zilizosababisha hofu kwa wananchi. Nashangaa kuchoma moto makanisa na kuiba mali kuna uhusiano gani na Muungano?,” alihoji Dk Shein.

Akieleza jitihada za Serikali katika kudhibiti hali hiyo, Dk Shein alisema walishabaini kutokea kwa hali hiyo mapema ndiyo maana yeye  kama Rais alifanya ziara katika visiwa vya Pemba na Unguja akiwaonya wananchi kujihadhari na uvunjifu wa amani.
“Mei 10 nilifanya ziara Unguja na Pemba nikawatahadharisha sana kuhusu kuvunjika kwa amani na kwamba, Serikiali haitavumilia mtu yoyote atakayevunja amani. Hilo lilikuwa onyo.”alisema.

Aliongeza kuwa kuna kamati ya Serikali iliyokutana na viongozi wa dini ili kusikiliza malalamiko yao na kwamba, hata Jeshi la Polisi limefanya kazi nzuri ya kurejesha amani katika hali yake.

Licha ya kutoa pole kwa wote walioathiriwa na vurugu hizo, Dk Shein alisema Serikali inafanya tathmini ya uharibifu uliojitokeza ili kuchukua hatua.

Dk Shein alifafanua kwamba, Seriklali yake haitaingilia shughuli za kidini isipokuwa kwa wale wanaotumia majukwaa ya dini kuhubiri siasa.

Rais Shein aliongeza kwamba  vurugu hizo zimeathiri Sekta ya Utalii inayotegemewa kwa asilimia 60 na Wazanzibari hivyo, akawataka wananchi wote kujihadhari ili kulinda uchumi wa nchi.

Katiba na Muungano
Kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba, Dk Shein alisema ameshiriki kikamilifu kuiunda Tume ya Katiba kwa kushauriana na Rais Jakaya Kikwete ambaye walikubaliana kuteua na kuweka viongozi wa Tume hiyo na kutaka wananchi kuisubuiri ili wakatoe maoni yao.

“Hii ni nafasi nzuri kwa Wazanzibari kutoa maoni yao ili tupate Katiba mpya. Hakuna kutishana wala chochote, kila mtu apate fursa ya kutoa maoni yake,” alisema na kuongeza:,

“Tusubiri wakati wa kutoa maoni, ni kweli Katiba imeruhusu uhuru wa maoni, lakini siyo kusema tu, tufuate utaratibu. Kwa sababu hata ukitoa maoni yako kwa sasa hayataandikwa wala kufanyiwa kazi.”

Wakati kundi la uamsho na makundi mengine visiwani humo wakiupinga Muungano waziwazi, Rais Shein alisema Serikali yake imekuwa ikifanya mazungumzo ya Muungano na upande wa bara kupitia Kamati ya watu sita iliyopo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo hujadili kero za muungano.

Alitaja vikao vitano ambavyo tayari vimeshafanywa na kamati hiyo ikihusisha viongozi wa Serikali kuwa ni pamoja na vinne vya Sekretarieti,  sita vya Kamati ya Utendaji,  vinne vya Makatibu Wakuu, vitatu vya Mapendekezo na kikao cha Waziri Mkuu na Rais wa Zanzibar, kilichofanyika Januari mwaka huu.

Katika vikao hivyo, alisema kuna mambo 12 ambayo yamekuwa yakijadiliwa hadi sasa ambayo ni pamoja na utafutaji na uchimbaji wa mafuta, ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Uvuvi katika Bahari Kuu na Ushirikiano na Taasisi za Nje.
Mengine ni ajira kwa Wazanzibari katika Serikali ya Muungano, uwezo wa Zanzibar kukopa nje, Kodi ya Mapato, Usajili wa vyombo vya Usafiri vya barabarani, ongezeko la gharama za umeme, Uharamia na Utekaji nyara Baharini, Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo na Utekelezaji wa Masuala ya Muungano.
“Kutokana na jitihada hizo naamini kabisa tutamaliza kero za Muungano na kuelekea kwenye katiba,” alisema Dk Shein.

Kiongozi JUMIKI afichua siri
Katika hatua nyingine, mmoja wa wasemaji wakuu wa Kikundi cha Mihadhara ya Kiislamu cha JUMIKI,  Sheikh Faridi Hadi Ahmed ametoa siri ya kikundi hicho akisema kuwa chanzo cha harakati zao ni baada ya Serikali ya Muungano kuleta Sheria ya Katiba inayowabagua Wazanzibari.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake Darajani Zanzibar, Sheikh Ahmed ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, alisema hata viongozi wa Serikali waliukataa Muswada wa Sheria ya Katiba, lakini, Serikali ya Muungano ikalazimisha ndiyo maana wao wameingia ili kuipinga.

“Vuguvugu la kupinga Muungano lilianza wakati wa Muswada wa Katiba ambao Serikali iliuleta. Serikali iliukataa na hata sisi Jumuiya za Kiislam tuliukataa, ilikuwa waurekebishe kisha waulete tena tuujadili, lakini wakauleta hivyo hivyo,” alisema Sheikh Ahmed na kuongeza:,

“Sheria hiyo ina upungufu mwingi. Kwa mfano, Kifungu cha Tisa kinazuia kujadili Muungano. Hata Rais alipozindua Tume ya Katiba alizuia kujadili uwepo wa Muungano. Sasa wanataka sisi tujadili nini?”

Sheikh Ahmed ambaye juzi alifikishwa  mahakamani Zanzibar akituhumiwa kuandamana bila kuwa na kibali, aliongeza kuwa Katiba ya Muungano na ya Zanzibar zimejaa utata kuhusu Muungano na hilo ndiyo wanalopigania."

“Katiba ya Muungano inasema Tanzania ni nchi moja, wakati Katiba ya Zanzibar inasema Zanzibar ni nchi. Sasa hapo tuelewe lipi? Halafu viongozi wetu hawasikilizi wananchi wanavyosema, hawasikilizi hata CD za mafundisho yetu? Kwanini Muungano usijadiliwe kwanza, kwa nini tuzuiwe?,” alihoji.

Amelilalamikia pia Jeshi la Polisi akisema  limeshiriki kuwatesa Waislam huku akiongeza kwamba hata yeye aliwahi kukamatwa na kuteswa na jeshi hilo mwaka 2004.

Sheikh Ahmed ambaye mwaka jana alichana nakala ya Muswada wa Katiba mbele ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ametetea ushiriki wa viongozi wa dini katika masuala ya siasa akisema hata Nyerere alikuwa hivyo.

“Kama Wakristo hawaruhusiwi kushiriki siasa ni kwa sababu dini yao inawaambia ya Kaisari mpe kaisari na ya Mungu mpe Mungu. Kwa Waislam hiyo haipo, Uislamu ni mfumo mzima wa maisha. Siasa ni neno la Kiarabu likimaanisha uongozi. Uongozi katika mambo yote.”

Akizungumzia suala la uchomaji wa makanisa wakati wa vurugu kama wanavyolalamikiwa, Sheikh Ahmed alikanusha madai hayo ila akaonya kuwa wakichokozwa watalipa kisasi.

“Mahubiri yetu hayachochei vurugu, ila tunasema yeyote atakayetuonea hatutakaa kimya,” alionya  na kuongeza:,

Kuhusu maisha yake wakati wa vurugu, alisema, "Ni kweli siku tatu za vurugu mimi sikulala nyumbani, ila sitaji nilipokuwa nikilala…nachukua tahadhari, unajua sisi hatuna jeshi wala silaha, ila linaloandikwa likufike litakufika tu. Heri mimi nife nikiwa jasiri kuliko kuacha taifa langu likiangamia.”

No comments: