BOB MAKANI AFARIKI DUNIA-Kuzikwa Shinyanga. - ANGA ZA KIMATAIFA

Latest

Monday, June 11, 2012

BOB MAKANI AFARIKI DUNIA-Kuzikwa Shinyanga.


Marehemu Bob Makani, enzi za uhai wake.
Katibu Mkuu wa kwanza wa Chadema, na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Bob Makani, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Agakhan jijini Dar es Salaam.
Bob Makani  ameshawahi kuwa Naibu Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania 

     Habari za kifo chake zimetolewa na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, ambaye amesema kuwa, Bob Makani amefariki dunia, baada ya kuugua kwa muda mrefu, na mwili wake umehamishiwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikopelekwa baada ya kuzidiwa ghafla.

    Kufuatia kifo cha mwasisi huyo wa chama hicho, sasa Chadema wamekatisha ziara za kuimarisha uhai wa chama zilizokuwa zikiendelea katika mikoa ya kusini mwa Tanzania.
Wakati huo huo, taarifa za familia zimesema Marehemu  utaagwa leo Dar es Salaam na utazikwa keshokutwa katika Kijiji cha Negesi, Wilaya ya Kishapu, Shinyanga.

Mtoto wa Marehemu, Mohamed Makani aliwaambia waandishi wa habari nyumbani kwa marehemu, Mbezi Beach kwamba mwili wa marehemu utaagwa leo katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
Alisema baada ya mwili huo kuagwa, utapelekwa katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere tayari kwa kusafirishwa kesho.
“Bado hatujafahamu mwili utaagwa kuanzia saa ngapi katika Ukumbi wa Karimjee, lakini tutaendelea kuwafahamisha wananchi baada ya mawasiliano ya wanafamilia,” alisema.

No comments: